Polisi Kusini mwa India wamesajili kesi ya ubakaji ambapo inaarifiwa mtoto wa shule mwenye umri wa miaka 6 alibakwa na wafanyakazi wawili wa shule moja maarufu mjini Bangaloer.Kisa hicho kinaarifiwa kutokea wiki mbili zilizopita.
Mtoto huyo alibakwa na mlinzi pamoja na mwalimu, lakini kwa sababu ya kuwepo walinzi wengi katika shule hiyo, polisi bado wanachukua muda kuchunguza mlinzi aliyehusika.
Polisi wanasema kuwa mtoto huyo alibakwa tarehe mbili Julai , lakini wazazi wake waligundua hilo siku chache zilizopita baada ya mtoto huyo kulalamika kuumwa na tumbo na kupelekwa hospitalini. Wakati huo mamia ya wazazi wameandamana nje ya shule wakivunja milango na kupiga mayowe kulaani tukio hilo.
Polisi tayari wamesajili kesi hiyo , lakini bado hawajamkamata mtu yeyote. Mwandishi wa BBC Andrew North mjini Delhi anasema kuwa tukio hilo ni la hivi karibuni kugonga vichwa vya habari nchini India.
Waziri mkuu Narendra Modi, ameahidi kupambana vilivyo na visa vya ubakaji, na udhalilishaji wa kijinsia , lakini unyanyasaji wa wanawake bado ni tatizo kubwa sana nchini humo.
Huku taarifa ya kubakwa kwa mtoto huyo zikijitokeza tu, mamia ya wazazi walikusanyika nje ya shule hiyo na kutaka hatua kuchukuliwa dhidi ya wasimamizi wa shule.
Mnamo siku ya Alhamisi mwenyekiti wa shule Rustom Kerawala alizungumza na wazazi ambapo aliomba msamaha na kuahidi kushirikiana na polisi katika uchunguzi.
source: BBC