Vikosi vya serikali Somalia vimefanikiwa kuidhibiti upya ikulu ya rais katika mji mkuu Mogadishu baada ya hapo awali wapiganaji wa kiislamu kuishambulia.Maafisa wanasema washambuliaji wapatao watano kutoka kundi la al-Shabab - waliuawa walipoingia katika eneo la ikulu hiyo.Washambuliaji hao wanadaiwa kulipua bomu lililotegwa kwenye gari karibu na langu kuu la Ikulu hiyo.Waziri wa habari na mawasiliano wa Somalia Mustaf Dhuhulow ameambia BBC kuwa tayari mmoja wa washambuliaji hao amekamatwa na anahojiwa na polisi.
Waziri Mustaf amesema, '' Walishambulia ikulu ya rais saa za jioni. Alikuwa watu washambuliaji watatu pamoja na dereva wao. Washambuliaji hao waliuawa lakini dereva wao alipata majeraha madogo na anazuiliwa na polisi na kuhojiwa. Walijaribu kuvamia Villa Somalia lakini wakakomeshwa. Tutawapa maelezo zaidi baadaye. Na tutaweza kutoa maelezo zaidi kwa raia wa Somalia na dunia nzima.''