Washambuliaji Thomas Ulimwengu na Mbwana Samata wa klabu ya TP
Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wanawasili nchini
keshokutwa alfajiri (Julai 16 mwaka huu) kwa ajili ya mechi dhidi ya
Msumbiji (Mambas).
Mechi
hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika (AFCON) kati ya
Tanzania (Taifa Stars) na Mambas itachezwa Jumapili (Julai 20 mwaka huu)
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ulimwengu
na Samata watawasili saa 12 asubuhi kwa ndege ya EgyptAir wakitokea
Tunisia ambapo timu yao ya TP Mazembe imepiga kambi kwa ajili ya mechi
za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imepiga kambi Tukuyu
mkoani Mbeya ikijiandaa kwa mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi
Mahmoud Ashour kutoka Misri.
Stars
itarejea jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa (Julai 18 mwaka huu) kwa
ajili ya mechi hiyo wakati Mambas nao wanatarajiwa kutua siku hiyo hiyo.
Mechi ya marudiano itachezwa kati ya Agosti 1 na 3 mwaka huu nchini
Msumbiji.