Mwanaume mmoja kutoka Ujerumani
anayeshikilia rekodi ya dunia ya kuwa mtu aliyetoboa zaidi mwili wake,
Rolf Buchholz amekatazwa kuingia Dubai.
Rolf Buchholz, ametoboa mwili wake mara 453 ikiwemo usoni mwake na ana pembe mbili juu ya paja la uso wake. Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 53 alikuwa ameratibiwa kuandaa onyesho katika klabu moja mjini humo. Bwana Buchholz alieleza kuwa maafisa wakuu katika uwanja wa ndege walihofia huenda alikuwa ni '' mchawi'' .Mtaalamu huyu wa tarakilishi alitambulika na kitabu cha rekodi za dunia cha Guiness, kama mwanaume aliyetoboa mwili wake zaidi duniani mwaka wa 2012.
Alieleza wanahabari wa Press News Agency kuwa hapo awali alikuwa amekubalika lakini baadaye akarejeshwa kabla ya kufika eneo la maafisa wa usafiri ndipo akarejeshwa katika ndege iliyokuwa ikielekea mjini Instabul Uturuki.
Onyesho lake katika mgahawa maarufu wa Irque le Soir ulioko katika hoteli ya Fairmont Hotel Dubai lilifutiliwa mbali.
Maafisa wa mgahawa huo wa Fairmont Dubai wamesema kuwa walifanya chochote kadri ya uwezo wao kumuingiza Buchholz nchini Dubai lakini hawakufua dafu.
Bwana Rolf amesema kuwa mizigo yake bado iko Dubai na aliapa kwenye mtandao wa kijamii kuwa hatarudi tena katika milki za Kiarabu.
Polisi na Maafisa wa usafiri wa ndege nchini Dubai hawajazungumzia swala hilo.