Mamia ya watu wamejitokeza nchini
Tanzania kumuaga marehemu Captain John Komba, mbunge na msanii maarufu
wa uhamasishaji aliyefariki siku ya Jumamosi.
Captain Komba
atakumbukwa kwa uhodari wake katika kuimba nyimbo za kuhamasisha
wananchi katika mambo mbalimbali hasa ya kisiasa kwa niaba ya chama
chake cha CCM.Mpaka anafariki alikuwa mbunge wa jimbo la Mbinga
Magharibi. Kando na siasa, Komba alishiriki katika uhamasishaji wa
jamii mfano wimbo wa ‘Mgeni’ uliokuwa ukitoa elimu juu ya ugonjwa wa
UKIMWI.Mwimbaji huyo pia alihamasisha uzalendo kupitia wimbo wake wa ‘Najivunia kuwa Mtanzania’
ingawa nyimbo zinazofahamika zaidi ni nyimbo alizokiimbia chama chake kukipigia kampeni na wagombea wake wakati wa uchaguzi.
Ingawa kikundi cha Tanzania One Theatre alichokuwa akikiongoza kilikuwa maarufu kuanzia miaka ya nyuma. Lakini umaarufu uliakua ulikua zaidi Captain John Komba alipotunga na kuimba nao nyimbo za kuomboleza kifo cha rais wa kwanza wa nchi hiyo Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1999.
Marehemu Captain Komba alizaliwa Machi 18 mwaka 1954 mkoani Ruvuma.
Na katika maisha yake aliwahi kuwa mwanajeshi kabla ya kustaafu na kujihusisha na siasa. Mwili wake umesafirishwa kuelekea kijiji cha Lituhi, mkoani Ruvuma ambako maziko yatafanyika siku ya Jumanne.